IJUE BIBLIA | KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU~01.

IJUE BIBLIA | KNOW THE BIBLE


KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU~01.










Bwana Yesu asifiwe…
Si watu wengi wenye kujua maana halisi ya Karama maana wapo watu wenye kulichanganya neno hili na neno kipaji. Kipaji na karama ni maneno mawili tofauti kabisa kwa sababu kipaji ni uwezo wa asili wa kimwili ndani ya mtu wa kutenda jambo fulani ,bali karama ni uwezo wa kiroho wa kutenda sawa sawa na muongozo wa Roho mtakatifu.
Hivyo basi,
Karama ni utendaji kazi wa Roho mtakatifu ndani ya mwamini aliyeokoka.
Kila aliyeokoka amepewa karama fulani kwa kufaidiana katika kuujenga mwili wa Kristo.
Katika fundisho hili zuri,tutajifunza katika vipengele vifuatavyo;
01. Tofauti kati ya ujuzi,kipaji na karama.
02. Tofauti kati ya wito na karama.
03.Aina za karama za Roho mtakatifu.
04. Sifa kuu za karama za Roho mtakatifu.
05. Faida za karama za Roho mtakatifu.
06. Utawezaje kuitambua karama yako?
07. Ni namna gani utachochea karama yako?
08. Ni kwa namna gani karama yangu itampendeza Mungu?
09.Changamoto za utendaji kazi katika kila karama.
01.TOFAUTI KATI YA UJUZI,KIPAJI NA KARAMA.
A)Ujuzi.(Skill)
Ni uwezo upatikanao kwa njia ya elimu fulani. Uwezo huu umuwezesha mtu kutenda au kufanya jambo fulani  kwa sababu ya elimu aliyoipata.
Hivyo,UJUZI ni uwezo wa kufanya jambo fulani katika ubora,au katika ufundi fulani kwa sababu ujuzi huo umepatikana kwa kusomea au kujifunza ( Capacity to do something well; technique, ability. Skills are usually acquired or learned, as opposed to abilities, which are often thought of as innate.)
Mfano 01; Mtu anaweza akaenda kusomea ufundi magari,kisha baadaye akawa ni fundi mzuri sana wa kutengeneza magari na hata kuyarekebisha. Ufundi huu uliopatikana kwa kisomo au mafunzo fulani ni ujuzi.
~Ujuzi hauji automatically yaani haumjii mtu moja kwa moja bali ni lazima akajifunze kwanza ndiposa awe mjuzi wa jambo fulani.
Mfano 02. Katika biblia tunaona wapo watu wengi tu waliokuwa na ujuzi wa kufanya mambo tofauti tofauti,mfano tunasoma; “ Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.“Mwanzo 4:20-21
Yabali baba yao,bila shaka alipitisha elimu juu ya ufugaji wanyama. Elimu hii juu ya ufugaji ilikuwa ni ujuzi wa namna ya kufuga wanyama. Katika jamii ya kiyahudi kulikuwepo namna ya kurithisha elimu ya ufugaji kutoka jamii moja hadi jamii nyingine. Mtazame pia Yubali baba yao wapigao kinubi na filimbi. Bila shaka elimu ya namna ya kupiga kinubi na filimbi ilifundishwa na kurithishwa. Na jambo hili tunaliona hadi katika kizazi cha Daudi,Daudi alikuwa ni mpigaji mzuri wa kinubi. Imeandikwa;
Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake.” 1 Samweli 18:10
Ukijaribu kuyatizama maisha ya baadhi ya wanafunzi wa Yesu,wengi wao walikuwa na ujuzi fulani katika maisha yao kabla ya kuitwa kuwa mitume. Mfano Petro alikuwa ni mvuvi,uvuvi huu wa Petro ulitokana na elimu ya awali kutoka kwa baba yake na jamii yake iliyokuwa wavuvi tangu awali. Alikadhalika ukimtazama mwinjilisti LUKA alikuwa na ujuzi mzuri tu wa utabibu kabla ya kuokoka katika misafara ya mtume Paulo. Tazama Wakolosai 4:14
▪Je ujuzi unahitajika katika kanisa la leo?
JIBU;Ujuzi unahitajika sana katika kanisa la leo. Maana si wote watakaokuwa ni wachungaji au si wote watakao kuwa ni waalimu kanisani bali wapo wengine watakaokuwa ni waamini wenye ujuzi wa mambo fulani yenye kulifaa kanisa liweze kusonga mbele kwa kujitosheleza. Mfano; Kanisa linahitaji wataalamu waliosomea namna ya kuendesha kitengo cha utawala ( Management) yaani jinsi ya kukontroo/ku-control matumizi ya pesa,jinsi ya kuwa na miladi endelevu ya kanisa,jinsi ya kuandaa mikutano,seminas,makongamano ( Maana huduma hizo zote zinahitaji pesa)
Tuangalie kanisa la kwanza lilivyoweza kushughulikia suala hili la utawala, ;
Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung’uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani
Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.” Matendo 6:1-4
Hapo,tunaona kabisa mitume walibidi waweke mambo ya kiutawala(management) ili kukidhi mahitaji ya kila siku ya watu wote. Kipindi mitume wanahudumu mezani pa Bwana,hapo ndipo pakatokea hali ya kutokutenda sawa kwa baadhi ya wajane wa kiebrania kusahauliwa katika huduma ya kila siku. Kumbe basi kanisa likikosa utawala(management team) halitaweza kutenda haki. Lakini pia kanisa la namna hii linaweza likakumbwa na manung’uniko mengi ya kihuduma za kila siku,maana wapo watu ambao watasahaulika katika baadhi ya mambo mbali mbali.
Kumbuka,Kazi ya utawala sio kazi ya mchungaji hapo kanisani kwa sababu kazi ya mchungaji ni kulihudumia lile neno na kuomba (Matendo 6:3-4).
Hivyo basi ,ujuzi unahitajika sana katika kanisa la leo,kumbuka tena watu wa utawala ni lazima wawe na ujuzi wa kuendesha mambo kanisani pasipo upendeleo wowote ule.
Lakini pia watu hawa wenye ujuzi wanatakiwa wawe ni watu safi rohoni,wasiwe na mawaa maana ikiwa watakuwa ni watu ovyo,yaani hawajaokoka wakamaanisha~basi waweza wakapendelea baadhi ya waamini hata kama wamejawa na ujuzi wa kutenda mambo. Tazama mfano wa wale saba waliochaguliwa katika kuongoza mambo ya utawala katika kanisa la kwanza (Matendo 6:3),Watu hawa walikuwa ni watu wema waliojawa na Roho mtakatifu…
ITAENDELEA…
Reactions

Post a Comment

0 Comments