IJUE BIBLIA | MAKOSA YA WATU WENGINE YASIKUFANYE NA WEWE UKOSEE

IJUE BIBLIA | KNOW THE BIBLE




MAKOSA YA WATU WENGINE YASIKUFANYE NA WEWE UKOSEE!




Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
Leo watu wengi wamemkosa Mungu kwa sababu ya makosa ya watu wengine. Eti kwa sababu mtu wako wa karibu kaanguka dhambini basi na wewe ndio uanguke uanguke dhambini!au ukosee eti kwa sababu na mwenzako kakosea! Nimejaribu kuliangalia jambo hili kwa ukaribu sana,na kugundua kwamba wengi wanaanguka dhambini kwa sababu ya watu wao wa karibu nao wameanguka.
Wale watu wa vyuoni wanaelewa ninazungumza nini mahali hapa. Maana wengi wao wanaanguka sana kwa sababu ya marafiki walionao karibu;hujawahi kuona mtu ni mzinzi kwa sababu tu rafiki zake ni wazinzi? Lakini leo ni lazima ujifunze kwamba hakuna haja wala sababu ya wewe mtu wa Mungu kukosea,kumkosa Mungu kwa kigezo cha makosa ya watu wengine.
 Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu;akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake.Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao.” Mwanzo 9:20-23
Hamu mwana mdogo wa Nuhu alikosea kuuona uchi wa baba yake Nuhu. Kitendo cha kuona “tupu ya baba yake” kilikuwa ni kibaya sana,Hamu alikuwa anao uwezo wa kutokukosea hivyo! Mbaya zaidi baada ya kuuona uchi wa babaye hakuchukua hatua nzuri ya kufunika kimya kimya,bali yeye alienda kuwapasha habari nduguze juu ya tupu ya babaye!!! Kosa la Hamu lingeweza kuwafanya Shemu na Yafethi kukosea,lakini akina Shemu wakatenda hekima.
Kumbe inawezekana makosa ya watu wengine yasikufanye na wewe ukakosea. Ebu Jifunze kwa Shemu na kwa Yafethi watu ambao walitenda vyema katikati ya makosa ya mtu mwingine. Kukosea kwa Hamu kulipelekea laana kwa mtoto wake Kanaani (uzao wa Hamu ulilaaniwa,kwa kosa moja tu)hapo unaweza kuona kwa kosa la mtu mmoja anaweza kukufanya nawe ukakosa hatimaye na wewe ukaingia kwenye laana ambayo kwa kweli haikuwa yako!
Shemu na Yafethi kana kwamba walijua hatari ijayo,gafla wakaona isiwe shida-wakajitanda vazi mabegani mwao na kumfunika mzee wao aliyekuwa uchi. Jifunze sana katika eneo hili,kwamba huna sababu za kumsikiliza weee! Mtu mkosa,badala yake chukua hatua mara moja ya kusawazisha kosa hilo,au la!basi kaa mbali na story zake za muda mrefu usije ukaingizwa katika hali ya kukosa na ukapokea laana za bure. Kumbuka,leo kuna watu wamekaa mkoa wa kukufanya ukosee na kumkosa Mungu,jitahidi kuwakwepa watu hao kwa gharama yoyote ile.
Mfano; mtu wako wa karibu anakujia gafla na anakushirikisha udhaifu aliouona kwa mtumishi wa Mungu ambaye kwa huyo mtumishi ni baba au mama yako wa kiroho. Nawe bila kujua unanogewa na mastory ya kumsema mtumishi wa Mungu kwa sababu mtumishi alijisahau akakaa vibaya. Kule kuendelea kumsema,ujue nyote wawili mtaangukia kwenye laana! Ni afadhali sana ukimbie hizo story,kisha utafute namna ya kumfunika mtumishi huyo kwa maombi asiendelee na tabia au hali aliyokuwa nayo.
Leo sisi wachungaji tunaangaika sana kuwaombea watu tukidhani kwamba wamelogwa,lakini kumbe sio kulogwa,bali ni laana wanazotembea nazo kwa sababu ya tabia zao kama tabia ya Hamu. Wewe unafikiri mambo yako yakiwa hayaendi basi umelogwa tu? Hapana mambo mengine unajiloga mwenyewe kwa makosa yako kwa sababu ya wengine waliokosea. Unanipata vizuri lakini? 
Ikiwa wewe ni kijana wa kiume au wa kike ni muhimu kujifunza kuwa makini hapo nyumbani kwenu unapoishi na ndugu zako wakubwa au wadogo zako. Unapoona fulani nduguyo kaiona aibu ya baba yako kwa sababu ya ulevi wake,basi wewe kataa kushiriki mazungumzo mabaya juu ya baba yako,bali wewe tafuta ufumbuzi wa tatizo hilo,jaribu kumfunika mzee wako na wale usiendelee kushiriki mazungumzo hayo ya kuufunua aibu ya mzee wako. 
Kumbuka;hata kama mzee wako anaitwa cha pombe wala hajaokoka,lakini ujue anayo nguvu ya kukutamkia laana na hiyo laana itakupata tu kwa sababu kwanza yeye ni mzazi wako,pili hiyo laana ina sababu ya kukupata maana umeufunua utupu au aibu ya baba yako kwa njia ya maneno ya kinywa chako pamoja na nduguyo,wote wawili mtalaaniwa hata kama mmeokoka. Ni muhimu kukaa kimya,na kufanya maarifa kihekima kuficha aibu ya mzee wako.
Hamu alipouona utupu wa babaye,alilaaniwa mwanaye Kanaani kwa makundi kabisa kwa maana maumivu ya laana yasingelikuwapo kama laana zile zingeenda kwake moja kwa moja,bali mtoto alipolaaniwa maumivu ya laana yalikuwa ni makubwa sana kwa sababu kizazi chake Kanaani ndicho kilichotembea kwenye laana hiyo,maana Kanaani alikuwa mtumwa wa Shemu. 
Hakuna sababu ya kuanguka dhambini eti kwa sababu ya wengine wameanguka dhambini. Fanya hivi;ikiwa wenzako wameanguka dhambini wewe usishiriki makosa yao,zaidi sana uwe tofauti nao,washauri na uwaombee.
Reactions

Post a Comment

0 Comments