ONGEZA UFAHAMU KUHUSU NDOTO PART 3

IJUE BIBLIA | KNOW THE BIBLE

ONGEZA UFAHAMU  KUHUSU NDOTO

1a
Mada: Mafunzo tupatayo kutoka kwa Daniel na Yusufu kuhusu kufasiri ndoto
Katika sehemu ya pili tuliangalia kuhusu mambo muhimu ya kujua kuhusu ndoto kama njia ya kukusaidia kufanya maamuzi.Karibu sasa tuendelee kwa kuangalia mafunzo tunayopata kutoka kwa Danieli na Yusufu katika kufasiri ndoto.
Mfano wa Danieli kupitia ndoto ya Mfalme Nebukadreza
Katika Daniel 2:1-2 imeandikwa ‘Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza, Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha. Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme’.
Ukisoma sura nzima ya pili utagundua kwamba mfalme aliota ndoto ambayo alipoamka aliisahau kabisa na hivyo akataka wasaidizi wake kwenye eneo hilo wampe tafsiri na akatoa amri wakishindwa kutoa tafsiri wote wataangaziwa, hii ni pamja na akina Danieli. Biblia inasema wale wasaidizi wake yaani waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo hawakuweza kutoa tafsiri kwani walitaka mfalme awaeleze ile ndoto kwanza, hivyo kwa kuwa walishindwa Mfalme akatoa agizo wote waangamizwe.
a
Danieli 2:12-13 imeandikwa Basi kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, akaona hasira nyingi, akatoa amri kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli. Basi ile amri ikatangazwa, na hao wenye hekima walikuwa karibu na kuuawa; watu wakamtafuta Danielii na wenzake ili wauawe’. Ndipo kufuatia amri hiyo Danieli akamwomba mfalme ampe muda wa kulifanyia kazi kwani imeandikwa ‘Basi Danielii akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonyesha mfalme tafsiri ile’ (Danieli 2:16).
Naam mstari huu ndio kiini cha ujumbe huu, ambapo nilitaka uone kwamba Danieli kwa kujua kwamba mwenye kutoa tafsiri sahihi ya ndoto ni Mungu ilibidi aombe muda kwa mfalme ili ndani ya muda huo aulize kwa Mungu mosi nini mfalme alichoota na pili nini tafsiri ya kile alichoota mfalme. Hii ni kutufundisha kwamba tunahitaji muda na nidhamu ya kuuliza kwa Mungu kila tuotapo ndoto.
Hivyo basi kila uotapo ndoto usitoke na tafsiri yako muulize Mungu atakupa tafsiri sahihi ya ndoto na si mwanandamu. Ukitaka kuthibitisha jambo hili washirikishe watu watatu tofauti ndoto uliyoota ndipo utajua kazi ya kufasiri ndoto si ya mwanandamu bali Mungu. Ukweli ni kwamba hata wale waganga na wabashiri endapo mfalme angewaambia ndoto aliyoota wangempa tafsiri za uongo ilimradi wasife.
Mfano wa Yusufu kupitia ndoto ya Farao – Mwanzo 41:1,8 imeandikwa ‘Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo’.
r
Kama ilivyokuwa kwa Nebukadreza Farao naye alioota ndoto iliyohusu wakati ujao kwa taifa lake na watu wake ila bahati nzuri yeye alipata neema ya kukumbuka ndoto husika. Naam pamoja na kukumbuka na kuwaeleza wasidizi wake hakuna aliyeweza kumweleza tafsiri ya ndoto ile ingawa ninaamini angetoa tishio la kuwaangamiza kama alivyofanya Nebukadreza lazima wangempa tafsiri za uongo. Sasa bahati nzuri kuna Msaidizi mwingine wa mfalme ambaye aliwahi kukaa gerezani pamoja na Yusufu alimweleza mfalme kwamba yupo mtu anaweza kumpa tafsiri ya ndoto yake.
Ndipo Yusufu akaletwa kwa Mfalme akitokea gerezani na mfalme akamwambia Yusufu, ‘Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri. Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani’ (Mwanzo 41:15-16). Baada ya jibu la Yusufu kwa Farao, Farao akamsimulia ndoto yote aliyoota.
Mpenzi msomaji, jibu la Yususfu kwa Farao linakufundisha nini ukikumbuka kwamba Yusufu alitokea gerezani? Jibu hili linatufanya tujue Mungu na Yusufu walikuwa marafiki, ufahamu wa Yusufu kuhusu Mungu ulikuwa ni wa kiwango kikubwa na alimjua Mungu anayemtumikia na zaidi nguvu zake na uwezo wake. Naam jibu hili  linatufanya tujue kwamba haijalishi Yusufu alikuwa na mapito magmu kiasi gani hakuruhusu mapito hayo yaharibu uhusiano wake na Mungu bali alidumu kulinda uhusiano huo maana alijua ndio ufunguo wa mawasiliano kati yao.
f
Kisha tunasoma punde mara baada ya simulizi Yusufu akamjibu Farao akamwambia ‘Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Wale ng’ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja’ (Mwanzo 41:25-26).
Naam sijui endapo umeona tofauti ya wazi kati ya kile kilichotokea kwa Danieli na Mfalme Nebukadreza na kati ya Yusufu na Farao. Danieli aliomba muda wa kwenda kuuliza kwa Mungu, lakini Yusufu hakuomba muda wa kwenda kuuliza kwa Mungu. Je tunajifunza nini? Kazi ya kufasiri ndoto ni ya Mungu, kuna mazingira maadam umekaa vizuri na Mungu, muotaji anaposimulia, Mungu analeta tafsiri ya ndoto husika moja kwa moja kwako, naam tafuta kufikia viwango hivyo.
 Somo litaendelea……
 Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA

Reactions

Post a Comment

0 Comments