IJUE BIBLIA | KNOW THE BIBLE
ONGEZA UFAHAMU KUHUSU NDOTO
Mada: Yasemavyo maandiko kuhusu ndoto
Ndoto ni moja ya njia muhimu sana ambazo Mungu anatumia mara kwa mara kusema na wanadamu. Naam ndoto ni lugha ya picha ambayo mtu anapewa maelekezo kwayo, ndani ya picha kunaweza kuwa na sauti au ujumbe fulani. Picha hizo zinaweza kuwa kwa njia ya tukio, hadithi, kisa, habari au uzoefu fulani. Binafsi sehemu kubwa ya maamuzi ambayo nimekuwa nikifanya tena bila kujutia uamuzi wangu msingi wake ni kile ambacho Mungu amekuwa akisema nami kupitia ndoto.
Kufuatia umuhimu, uzito na upana wa jambo hili nimeona ni vema kuandaa ujumbe huu ambao najua kwa sehemu utajibu baadhi ya maswali ya wasomaji wengi juu ya ndoto na muhimu zaidi utakuwa ni mwongozo muhimu kwako wa kukusaidia kuelewa ujumbe unaobebwa kwenye ndoto na hivyo kukusaidia kufanya maamuzi sahihi.
Kumbuka kwamba lengo la Mungu kukuletea ndoto ni ili kukuongoza katika njia sahihi ya kueiendea na hivyo kulitumikia vema shauri lake uwapo duniani. Watu wengi ukiwauliza utasikia wakisema nimekuwa nikiomba kwa muda mrefu sana lakini sijaona Mungu akijibu, ukimuuliza hujawahi kuota ndoto yoyote kuhusiana na unachokiomba anakuambia mara kadhaa nimeota lakini ni ndoto tu sioni majibu ndani yake.
Ndio watu wengi wana mtazamo huo, wanataka wakiomba wasikie Mungu anawajibu kwa sauti au waone mtumishi (Nabii) anasema kuhusu mambo yao moja kwa moja. Watu hawa wasichojua ni kwamba kuisikia sauti ya Mungu waziwazi kama mtu asemavyo ana kwa ana na mwenzake ni hatua inayohitaji ufahamu wa kutosha juu ya Mungu anavyosema, muda na nidhamu ya kusikiliza, kufuatilia na kuuliza ili kuelewa alichosema huku ukiwa na msingi mzuri wa uaminifu katika neno la BWANA kwenye maisha yako (Hesabu 12:1).
Pengine niseme ili umsikie Mungu akisema ana kwa ana si kazi nyepesi kama unavyoweza kusema na baba yako mzazi, kwani kama ndoto ambayo ndani yake anakuletea picha huelewi, usidhani sauti yake utaielewa, maana hasemi kwa namna unayotaka wewe bali sawasawa na mapenzi yake, fuatilia majibu ya Yesu kwenye hoja za wanafunzi na wayahudi ndipo utaelewa ninachokisema, naam hata walipomuuliza kwa faragha afafanue kile alichosema nao awali bado aliwajibu kwa namna ambayo kumuelewa ilihitaji ufunuo wa ziada.
Jambo muhimu ni kwamba Mungu wetu anatufahamu vizuri yeye husema nasi kwa njia ambazo anajua itakuwa ni rahisi kwetu kuzielewa, naam usikimbilie masomo ya shule ya sekindari wakati ya shule ya awali (msingi) hujamaliza na kufaulu. Jifunze kwanza kuandika a, e, i, o, u ndiyo utaanza kujua kuumba na kuandika maneno.
Biblia kwenye kitabu cha Ayubu 33:14 inasema ‘Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika NDOTO, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani’.
Hapa Biblia inatueleza kwamba ndoto ni NJIA ambayo Mungu anatumia kusema na wanadamu. Haina maana ndani ya ndoto lazima usikie sauti ikisema, bali picha, kisa, tukio unaloona kwenye ndoto ni ujumbe tosha kwako kutoka kwa Mungu. Mara kadhaa ndani ya ndoto unaweza pia kusikia sauti ingawa si ndoto zote huambatana na sauti. Ndoto huja pale mtu anapokuwa amelala usingizi na hili lina maana, mtu anahitaji muda na mazingira bora ya kulala ili Mungu aweze kusema naye kwa njia hii.
Katika Hesabu 12:6 imeandikwa ‘Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, NITASEMA NAYE KATIKA NDOTO’. Ndiyo, Mungu husema kupitia ndoto, kwa kuwa ndoto ni lugha ya picha tena rahisi ya mawasiliano kwa yeye kufikisha ujumbe wake na hivyo kumsaidia mtu aelewe mpango wake (Mungu) kwenye maisha yake na hivyo kufanya maamuzi muafaka.
Mathayo 27:19 ‘Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake’. Hii ina maana Mungu alitumia ndoto kusema na mke wa Pilato juu ya Yesu. Naam maamuzi aliyochukua Pilato kuhusu kumsulubisha Yesu msingi wake ulikuwa ni ndoto za mkewe na ndio maana kwanza alitaka kuzuia Yesu asisulubiwe kwa kuuliza amfungulie nani kati ya Yesu na Baraba, akifikiri watamchagua Yesu kwa sababu ya matendo ya Baraba, alipoona ameshindwa ndipo akasema sina hatia juu ya damu hii (Mathayo 24:17,27).
Matahayo 1:20 ‘Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu’. Naam Mungu alitumia ndoto kuleta jibu kwa Yusufu juu ya mashaka yake kuhusu ujauzito wa Mariamu na zaidi kama mwenza wake. Hapa tunajifunza kwamba ndani ya ndoto malaika wanaweza kutumwa ili kusema nawe moja kwa moja, kwa hiyo badala ya kuwaona kwa macho ya kiroho unawaona katika ndoto.
Mathayo 2:12-13 ‘Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize’. Uamuzi wa wa Mamajusi kurudi kwa njia nyingine ni matokeo ya ndoto waliyoota, naam uamuzi wa Yusufu kwenda Misri ni kufuatia maelekezo aliyopewa kupitia ndoto.
Naam, yapo maandiko mengi sana ambayo ningeweza kuayaandika hapa lakini kwa haya machache naaamini umeanza kuona umuhimu na nafasi ya ndoto kwenye maisha yako, usizipuuze ndoto maana ndani yake kuna ujumbe muhimu kutoka kwa Mungu. Mungu akubariki, tutaendelea na sehemu ya pili…
Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.
0 Comments