DOMINIKA YA 5 YA PASAKA MWAKA B

MJUE MUNGU ILI UWE NA AMANI | IJUE BIBLIA



DOMINIKA YA 5 YA PASAKA MWAKA B

“Kaeni ndani yangu nami ndani yenu, alleluia” Yn 15:4

Ni hamu ya mwanadamu kujipatia ukamilifu na kuishi milele. Ukamilifu huo wa uzima upo katika Yesu Kristo Mfufuka aliye Mzabibu wa kweli. Tuongozwe na neno la Kristo “kaeni ndani yangu nami ndani yenu.”

Yesu hakuwa wa kwanza kutumia picha ya mzabibu, ‘Nami nilikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje basi kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu?(Yer 2:21, Isa 5:1-4). Waisrael walijipambanua kama zabibu pori zisizozaa na hivi Mungu aliye Mkulima aliwaharibu na kupanda zabibu nyingine (Isa 5:5-7). Kristo Mzabibu mpya analeta matunda yasiyokuwapo bado yaani haki, uaminifu na upendo. Zabibu hizi zilipandwa siku ya Pasaka Baba alipomfufua Mwana kutoka kwa wafu.

‘kaeni ndani yangu nami ndani yenu’ maana yake ni kuwa na uzima. Sote tunao msukumo wa ndani kabisa wa kuishi. Ndio maana tunatunza uhai bila kujali gharama, iwe ni chakula, mavazi, malazi, matibabu na hivi tunafanya kazi daima kusudi tuwe na uzima. Uzima wetu wa kidunia ni lazima uakisi uzima wa milele katika Mungu. Kristo ndiye Bwana wa uzima (Yn 11:25). Kwa kuzaliwa, kuteswa, kufa na kufufuka kwake ametupatia huo uzima, basi tuishi ndani yake naye ndani yetu. Tuisikie sauti yake na tufuate maelekezo yake. Maisha yetu yajae uzima utokanao na huduma ya kimapendo kwani ‘tunazaliwa ili kupenda, tunaishi ili kupenda, tunakufa ili kupenda zaidi’ (Mt. Yosefu Cafasso). Ndipo basi somo II (1Yoh 3:18-24) linatuasa ‘tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli’.. Je, umewahi kupenda? yapi matokeo yake? ulipopenda ulipata furaha au ulichuma usaliti na maumivu? Usikate tamaa PENDA, PENDA, PENDA.
 
- Kumbuka, Mungu anatupenda sana, hivi tufurahi kwa vile tunapendwa na Bwana
- Kumbuka, Mungu anayetupenda anataka nasi tupendane.
- Kumbuka, Mungu ni Upendo, jirani yangu ameumbwa kwa sura/mfano wa Mungu, kwa hiyo jirani yangu ni upendo.

Mzabibu una shina na matawi, Kristo ndiye shina nasi ni matawi, anaendelea kuzaa matunda kutoka kwa Mungu Baba kwa njia yetu na hilo litawezekana ikiwa sisi matawi tutabaki tumeungana na Yesu shina. Amesema ‘Yeye akaaye ndani yangu nami ndani yake huyo huzaa sana’. Siku ya Matawi tulishika matawi ya kijani kabisa, leo yameishakauka. Tawi likitoka kukatwa huonekana kijani lakini haliwezi kuzaa tena. Nasi pia nje ya Yesu hatuna uhai, tunanyauka na kufa.
 
Hata hivyo bado kuna miti yenye matawi yasiyozaa chochote japo yangali bado kwenye shina. Hawa ndio sisi tunaojiita wakristo, tumo kwenye rejista za Kanisa za ubatizo, Kipaimara na Ndoa lakini hatuzai matunda yaani hatuiishi Injili ya Kristo Mfufuka. Yesu amesema ‘kila tawi ndani yangu lisilozaa Baba huliondoa’ anamaanisha hatari ya kukataliwa mbele za Mungu ipo hata kwetu licha ya kuonekana safi kwa nje, ‘si kila aniambiaye Bwana Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni bali ni Yeye ayatendaye mapenzi ya Mungu’ (Mt 7:21). Wanaoomba rushwa, wasiotenda haki na kuonea watu, wanaowanyanyapaa wagonjwa na kuwadhulumu mali za wanyonge, wanaonyanyasa akina mama kwa vile hawawezi kushtaki popote, wanaodanganya na kughushi nyaraka mbalimbali wengi wao ni wakristo wenzetu. Hawa ni matawi ndani ya mzabibu lakini hayazai, yamekauka.

‘Kaeni ndani yangu nami ndani yenu, alleluia…’ hili nalo neno!! kukaa ndani ya Yesu na Yesu kuwa ndani yetu ni neno zuri tena la faraja kubwa. Walio ndani ya Yesu hawana hila na jamii inawapenda na kuwapokea. Tazama Mt. Paulo katika somo I (Mdo 9:26-31) anavyoogopwa na wakristo, wanamuona adui sababu alilitesa Kanisa akawa tawi bovu lililokauka, sasa ameongoka na bado haaminiki. Ilibidi Barnaba aingilie kati kumtambulisha kwao ndipo walipompokea kama mwenzao. Je, mimi na wewe tunapokelekaje mbele ya wenzetu? Unaponiona unajisikiaje? Unapata furaha au hapana? Kama uwepo wetu kati ya wenzetu unaleta baraka, amani na faraja heri yetu, sisi ni matawi yenye kuzaa na Baba atatusafisha tuzidi kuzaa. Lakini kama muonekano wetu mbele ya wenzetu ni makwazo na machukizo halafu sisi ni matawi mabovu na hayo Baba huyaondoa kwa wakati wake, ‘ shoka limekwishawekwa penye mashina ya miti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa katika moto usiozimika’ (Mt 3:10). 

‘Kaeni ndani yangu nami ndani yenu, alleluia,’ kukaa ndani ya Yesu kunahusisha imani katika Yesu Kristo na katika kuzishika amri zake. Somo II linafafanua kwamba ‘naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake; na katika hili tunajua kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa’. Basi na tuzishike amri zake, tupokee sakramenti na tusali.

‘Kaeni ndani yangu nami ndani yenu, alleluia’, kukaa ndani ya Yesu kunahusisha sadaka na majitoleo. Ukristo ni dini ngumu, ni kujitoa, kujisadaka na wakati mwingine ni kutokueleweka. Ukristo sio simu za mikononi hapana! Tusirahisishe mambo, mbinguni hatuendi kwa ujanjaujanja. Hakuna dini kwenye simu za mikononi. Wengi tumeacha kuja kusali huku tukibadilishana pepo na baraka pasipo hofu, utasikia tuma ujumbe huu kwa watu 10 utaingia mbinguni, au tuma ujumbe huu kwa watu 15 halafu kesho jioni utapata fedha, ukidharau utapata mkosi. Mbingu sio mchezo. Yesu amesulibiwa na kuchomwa mkuki ubavuni kwa ajili yetu halafu wewe eti utume ujumbe kwa watu 10 tena message zenyewe za promosheni tu ya cheka toka Vodafone halafu uingie mbinguni au upate mafanikio katika maisha yako! Hapana, fanya ujanjaujanja mahali pengine lakini sio katika mambo ya Mungu. Ishi ndani ya Yesu na Yesu ndani yako utajipatia ukamilifu wa uzima wako.

‘Kaeni ndani yangu nami ndani yenu, alleluia’ tunakaa ndani ya Yesu kwa njia ya sala na ibada. Katekisimu inafundisha kwamba sala lazima ibubujike kutoka chemchemi halisi ya Roho Mt anayewezesha neno la Mungu, liturjia ya Kanisa na fadhila za kimungu. Familia zinaposali zinakuwa mfano mzuri wa mzabibu wa Bwana. Kwamba baba, mama na watoto wanaishi kwa umoja ni neno zuri. Kitendawili… Tatutatu mpaka Ulaya! Kitendawili… nina watoto wangu nikimtoa mmoja hatuli ugali! Familia imetelekwa juu ya mafiga 3 ya baba, mama na watoto katika Mungu. Kama vile harusi ya Kana ilivyomwalika Yesu na kupata neema ya kuongezewa divai hata familia zetu zinapomwalika katika sala zinapata neema mbalimbali kulingana na mahitaji. 
Je, tuliwekaje swali hili? Ni nani mwenye matatizo, ni watoto wa siku hizi au wazazi wa siku hizi? Ni vijana wa siku hizi? Au ni wazee wa siku hizi? mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Hii ina maana kuwa maisha ya mtu hutegemea aina ya malezi anayopata. 
Mtoto Judith mwenye miaka 4 tu alimwambia mama wa jirani, ‘mama yangu hajui kulea watoto’. Mama jirani akashangaa na kuuliza ‘kwa nini unasema hivyo?’ Mtoto akajibu ‘ni kwa sababu huwa ananilazimisha kulala jioni wakati sina usingizi na kunilazimisha kuamka asubuhi wakati nina usingizi’. Jirani akajisemea moyoni ‘watoto wa siku hizi bwana!’ 
Msemo huu una maana kwamba watoto leo wamekuwa changamoto kwa wazazi, ni kama kero hivi, ni shida. Watoto leo tunaongea lugha ambazo wazazi wetu hawazielewi, Kiswahili si Kiswahili, Kiingereza si Kiingereza. Wakibaki nyumbani peke yao halafu wakaja rafiki zao huvuruga kila kitu. Yaani inakuwa paka ametoka hivi panya wanatawala. Hufungua Tv na radio sauti za juu utadhani mtaa mzima wanahitaji hilo. Hawasomi hadi walazimishwe kufanya mazoezi ya shule. Vijana tulio wengi hatupokei maonyo na maelekezo ya wazazi/walezi badala yake tunapokea maelekezo mitandaoni. Hatupishi wakubwa kwenye viti vya mabasi na tunawadharau wakubwa hao. Vijana ‘kaeni ndani yangu nami ndani yenu’ mtazaa zabibu njema na sio zabibu pori.
 
Imenenwa pia, ‘wazazi wa siku hizi bwana!’ Eti wanatofautisha chumba chao na cha watoto kwa mapazia tu, kwamba wanawaogopa watoto wao, wanawabembeleza tu na kuwapa chochote wanachokitaka. Hawawaonyi juu ya mavazi yao wala juu ya tabia na mwenendo wao. Oh, wazazi wa siku jamani, hawana umoja na kila mmoja anahusiana na watoto kivyake. Mama anamuuliza mtoto ‘baba yako amekupa sh. ngapi? Mtoto anajibu 5000 mama anaanza kumlaumu baba mbele ya mtoto na kunyang’anya hela hiyo’. Wakati mwingine mtoto huweza kumtisha mama yake na mama anakosa nguvu na kuwa mpole, kwamba mtoto huyu atamsema mama kwa baba kuhusu uncle anayekuja nyumbani baba akisafiri. 
Mtoto ni malezi, ili wali uupate sharti upike mchele, na mchele uupete, mpunga na chuya vitoke.. ndio ngozi iwahi ingali maji, malezi ni jambo kubwa, ingawa elimu ni bora hekima ni bora zaidi, tujipe moyo, tukazane, naye Mungu atusaidie ili neno hili litukae, ‘kaeni ndani yangu nami ndani yenu, allelluia!!’

By Fr. Patrick Njau C.S.Sp
Paroko Parokia ya Igoma-Mbeya
Reactions

Post a Comment

0 Comments